Sunday, March 13, 2011

ASKOFU KAKOBE ANASEMAJE KUHUSU BABU WA LOLIONDO?

Askofu Mkuu wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF), Zachary Kakobe jana akihubiri katika kanisa lake lililopo Mwenge jijini Dar es Salaam alisema uwepo wa mchungaji Mwasapile unatishia vituo vya maombezi vinavyofurika mijini kubaki vitupu kutokana na watu kukimbilia Loliondo.

Kakobe alisema Watanzania wengi wanapenda uwongo kuliko ukweli na kutahadharisha kuwa kutokana na kuwepo mtu huyo watu hawatasubiri tena maombezi bali watapukutika kwenda Loliondo. “Hofu yangu iko katika vituo vya maombezi vilivyofurika mjini, wakati huu vitabaki tupu, watu wataenda Loliondo na hawatasubiri tena maombezi,”alisema Kakobe na kuongeza : “Tukisema tusubiri serikali ama TFDA ituthibitishie itakuwa ngumu maana kila mmoja anatia bidii kama polisi na wengine”. 
Picture
Askofu Zakaria Kakobe

Alisema kanisa lake litaendelea kuwepo na kamwe haliwezi kutikiswa na Loliondo na kujigamba kuwa wanaweza kumsambaratisha mchungaji huyo.

Kakobe alieleza kuwa kwake yuko muhubiri wa Injili iliyo hai na ambayo iko ndani ya Biblia huku akikumbusha mtu aliyemwita 'Babu wa Tegeta' ambaye alijitokeza miaka ya nyuma na kudai kuwa anatibu UKIMWI ambaye alisema walimsambaratisha. Kakobe ambaye alitumia muda mwingi kunukuu vifungu mbalimbali vya Biblia, alisema mfumo wa uponyaji wa Mungu umeshafunuliwa na kwamba kwa sasa hawahitaji Mungu yeyote atoe ndoto.

“Hizi ni nyakati za mwisho, unatakiwa kuchagua kanisa ambalo utaongozwa katika haki na si kupeperushwa kama karatasi,”alisema Kakobe huku akishangiliwa na waumini wake. Aliwatahadharisha waumini wake akiwataka kuwa makini na mchungaji huyo huku akimtuhumu kwa kudai kuwa anatumia nguvu za giza.

“Kama umesikia mtu fulani anafanya maombezi la kwanza la kujiuliza je ameokoka kwa sababu Mungu hatendi kazi na watu ambao hawajaokoka, lazima awe anahubiri Injili,”alisema. Askofu huyo alitumia ibada hiyo kuwahamasisha waumini wake kumpinga mchungaji huyo kwa maombi huku akitamka: "Kanyaga Babu wa Loliondo, sambaratisha babu wa Loliondo, kazi za babu saga."

Kakobe alikwenda mbali zaidi na kumfananisha mchungaji huyo na mganga wa kienyeji huku akijigamba kuwa hata kanisani kwake watu waliokuwa na UKIMWI walipona.“Tusibabaishwe na UKIMWI, hapa tumeombea watu wamepona UKIMWI na vithibitisho vya vyeti vipo,” alisema Kakobe na kushangiliwa na waumini wake ambao baadhi yao walisikika wakisema, "tupo."

Kakobe alisema hata kama mtu huyo angekuwa anatibu kwa shilingi 1 kwenye Neno la Mungu haikubaliki na kueleza kuwa maandiko yanasema, 'mmepewa bure toeni bure.'

No comments:

Post a Comment