Hivi karibuni ameibuka mtu (mchungaji) na kujitangaza kuwa anatibu (anaponya) magonjwa yote sugu na hata yale ambayo matabibu wamedai hayana tiba. Babu huyu anayeishi maeneo ya Loliondo mkoani Arusha amevitikisa vyombo vya habari vya kitaifa na hata vile vya kimataifa. Kwa ufupi ni kwamba huyu “mponyaji” amejipatia umaarufu wa ghafla. Mambo mengine yamesahaulika kwa muda na mada imekuwa ni “mchungaji wa Loliondo.” Watu kutoka pande mbalimbali za ndani na nje ya nchi wamekuwa wakimiminika kwenda kupewa tiba na babu huyo mwenye fani ya uchungaji.
Wale ambao tayari wamefika huko Loliondo wanadai tiba yenyewe ni dawa itokanayo na mti ambao babu huyo alioteshwa kwamba ungekuwa jibu la matatizo ya kiafya ya dunia miaka kadhaa iliyopita. Mgonjwa hupewa kikombe kimoja tu cha dawa hiyo na hupona mara! Vidonda vya tumbo, kansa, kisukari, UKIMWI na magonjwa mengine sugu inadaiwa kwamba hupona mara moja baada ya kupewa dawa hiyo. Kinachowashangaza na labda kuwavutia wengi ni bei ya dawa hiyo. Kwa shilingi 500 (ndiyo, mia tano) tu magonjwa yako yote yanapona. Maajabu, si eti eh?
Wakati nikitafakari mambo haya na kuona namna watu wanavyomiminika kwenda Loliondo nimegundua kwamba jamii yetu ya Watanzania iko mahututi – inaumwa. Kwa miaka mingi sasa tumekuwa tukisubiri “tabibu wa ukweli” wa magonjwa yetu lakini hajapatikana. Matabibu ambao tumekuwa nao kwa miaka mingi sasa wamekuwa wakitutibu kwa nje tu. Wamekuwa wakitibu dalili za magonjwa yetu badala ya kuponya magonjwa yenyewe. Magonjwa ambayo jamii yetu imekuwa ikiteseka kwayo ni sugu. Watanzania tumeugua tangu mwaka 1961 hadi leo – miaka 50!
Tuna gonjwa sugu la UMASKINI. Tangu 1961 (au kabla?). Sugu. Tuna gonjwa la UJINGA. Hili nalo limeua watu wetu wengi sana. Hatujawahi kulipatia tiba. Tuna gonjwa la UFISADI. Hili ni gonjwa hatari sana. Wameugua viongozi wetu karibia wote – walio juu na hata wale wa chini. Hoi bin Taaaban. Gonjwa la CHUKI. Hili nalo limeua wengi hapa nchini kwetu. Tunachukia mtoto wa jirani yetu akifaulu mtihani wa darasa la saba. Tuna gonjwa la UVIVU. Hili ni gonjwa la kutopenda kufanya kazi. Tunakaa tu na kupiga porojo – watu wanakufa. Zinduka
No comments:
Post a Comment